MCHEZAJI MWINGINE WA 3 WA BARCA KORTINI UKWEPAJI KODI!
WAENDESHA MASHITAKA wa huko Spain wamefungua Kesi dhidi ya Beki wa Mabingwa wa Nchi hiyo Barcelona, Adriano Correia, kwa tuhuma za ukwepaji Kodi ikiwa ni Wiki chache tu kabla Staa wa Klabu hiyo Lionel Messi kuanza kusikilizwa kwa Kesi yake ya Mashitaka kama hayo.
Adriano anakuwa Mchezaji wa 3 wa Barcelona kukumbwa na Kesi za Ukwepaji Kodi katika kipindi hiki.
Kwa mujibu wa Waendesha Mashitaka, Adriano, Mchezaji kutoka Brazil, alikwepa kulipa Kodi ya Euro 646,086 kati ya Miaka 2011 na 2012 aliposhindwa kubainisha Mapato yake kutokana na Haki Miliki zake za Picha na Matangazo yake.
Licha ya Adriano kulipa Deni hilo baada ya kufunguliwa Mashitaka, Mchezaji huyo ataendelea na Kesi yake na imedokezwa atapigwa Faini.
Mkasa huu umekuja wakati Messi na Baba yake Mzazi, Jorge, wakijitayarisha kutinga Mahakamani wakidaiwa kukwepa kulipa Kodi ya Euro Milioni 4.16 kwenye kipindi cha 2007 na 2009 iliyotokana na Haki Miliki za Picha na Matangazo ya Messi.
Messi amekana Mashitaka yote akijitetea ni Baba yake ndie anaesimamia masuala yake yote ya Mapato yake.
Ingawa Messi amelipa Fedha zilizodaiwa, Kesi yake bado ipo na itaendelea hapo Mei 31 wakati Messi mwenyewe atakapotinga Kortini kutoa ushahidi.
Mwezi Januari, Mchezaji mwingine wa Barcelona, Javier Mascherano, alipigwa Kifungo cha nje cha Mwaka Mmoja na kutwangwa Faini ya Euro 816,000 kwa ukwepaji Kodi ya Euro Milioni 1.5.
0 comments:
Post a Comment